Friday, 11 April 2014

MFAHAMU MSHINDI WA TUZO YA HALL OF FAME 2014

    Baraka A. Dishon ni mwandishi wa mashairi na vitabu kwa lugha ya kiswahili na kiingereza, Alianza kazi ya uandishi wa mashairi na vitabu akiwa anasoma shule ya msingi, pia  alijifunza uandishi kupitia kwa Mama yake Mzazi ambaye alikuwa mwalimu wa shule ya msingi na mwandishi wa mashairi mbali mbali.
Baraka A. Dishon alianza kujulikana kupitia mashindano ya UMITASHUMTA akiwa darasa la tano mwaka 1998 katika shule ya  msingi Sambanyasoko, iliyopo wilaya ya Tarime mkoani Mara, aliposhiriki katika mashindano ya uandishi wa mashairi na kufanikiwa kuingia ngazi ya mkoa na baadae ngazi ya kitaifa ambapo alishindwa kushiriki ngazi ya kitaifa kutokana na kukosa wafadhili.
    Mnamo mwaka 2001 alijiunga shule ya sekondari Misonga ambapo aliendeleza kipaji chake cha uandishi wa mashairi alikuwa akitunga mashairi yenye mada tofauti kwa ajili ya kuwaelimisha wanafunzi wenzake nyakati za Asubuhi wakiwa Mstarini wakisubiri kuingia madarasani.
    Mwaka 2004 akiwa mwanafunzi shuleni hapo alipata nafasi ya kwenda kushiriki mashindano ya uandishi wa mashairi Nairobi nchini Kenya, mashindano yaliyohusisha shule zilizo chini ya Madhehebu ya kikristo Afrika Mashariki, alifanikiwa kuibuka mshindi wa tatu(3) katika uandishi wa mashairi na kushika nafasi ya kwanza kama Mwandishi bora wa Makala ya kiingereza.
   Mwaka 2005 alijiunga na shule ya Ufundi Musoma kwa ajili ya  kidato cha tano na sita katika mchepuo wa HKL, akiwa shuleni hapo alishiriki mashindano ya uandishi wa mashairi  yaliyoshirikisha shule za sekondari ikiwamo shule ya wasichana Kowaki na aliibuka mshindi wa kwanza kwa uandishi wa mashairi na makala.

   Mwaka 2006 alishiriki mashindano ya mazingira yaliyoratibiwa na ofisi ya Makamu wa Rais na alifanikiwa kushika nafasi ya kwanza na kutwaa tuzo ya mwandishi bora wa mazingira mwaka 2006.
   Mwaka 2009 aliajiriwa kama Mwalimu katika shule ya sekondari Morombe akiwa shuleni hapo kama mwalimu alifanikiwa kuanzisha kikundi cha wanafunzi wanaoandika mashairi kinachoitwa UJIKO GROUP.
  Mwaka 2011 alijiunga na chuo na chuo kikuu Mzumbe  kampasi ya Mbeya kusomea Shahada ya Sheria, akiwa chuoni hapo amefanikiwa kuandika mashairi mbali mbali ikiwamo shairi linalojulikana kwa jina la "Tatizo nini wanasheria". 
  Mnamo Aprili 2014 alipata taarifa ya mashindano ya tuzo za Hall of fame akiwa darasani  anandaa shairi kwa ajili ya sherehe ya Siku ya Wanasheria iliyofanyika tarehe 5 Aprili 2014 chuo kikuu Mzumbe kampasi ya Mbeya.
  Baraka A.Dishon aliibuka mshindi wa tuzo za Hall of fame katika kipengele cha mwandishi bora wa mashairi anayechipukia (Best Young Writer 2014) na kutwaa tuzo ya Shaaban Robert.

No comments: