Tuesday, 6 May 2014

RIPOTI YA CAG YACHACHAFYA CCM, CHADEMA

Bunge la Bajeti linaanza vikao vyake kesho mjini Dodoma na moja ya kazi zake zitakazovuta hisia za wengi ni Ripoti ya Mwaka 2012/13 ya Mashirika ya Umma na Taasisi za Serikali itakayowasilishwa na Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG). 
Pia, ripoti hiyo itakayowasilishwa keshokutwa baada ya kumalizika kwa kipindi cha maswali na majibu, kwa mara ya kwanza itahusisha hesabu za vyama vya siasa nchini ambavyo kwa muda mrefu vimekuwa vikidaiwa kutofanya ukaguzi wa hesabu zake.
Mawaziri waliotajwa katika ripoti hiyo ya 2012 ya CAG na hivyo kushinikizwa kujiuzulu ni William Ngeleja (aliyekuwa Nishati na Madini), Omar Nundu (Uchukuzi) na Naibu wake Athuman Mfutakamba. Wengine ni Mustafa Mkulo (Fedha), Ezekiel Maige (Maliasili na Utalii), Dk Hadji Mponda (Afya na Ustawi wa Jamii) na naibu wake, Dk Lucy Nkya pamoja na Dk Cyril Chami (Viwanda na Biashara). 
Vyama vya siasa
Ripoti hiyo pia itakuwa mwiba mchungu kwa vyama vya siasa ambavyo mwaka jana kwa nyakati tofauti Zitto alivinanga kuwa hesabu zake hazikaguliwi.
Zitto alifikia hatua ya kusimamisha ruzuku ya kila mwezi kwa vyama hivyo hadi vitakapowasilisha taarifa za ukaguzi wa fedha za umma tangu mwaka 2009 kwa Msajili wa Vyama vya Siasa. Katika maelezo yake, Zitto alisema tangu mwaka 2009 vyama tisa vya siasa vinavyopewa ruzuku na Serikali vilipata jumla ya Sh67.7 bilioni, lakini havijawahi kuwasilisha taarifa za ukaguzi wa ruzuku kwa Msajili kama inavyopaswa kisheria.
Madai hayo ya Zitto yaliibua malumbano makali kati yake na viongozi wa vyama hivyo, kikiwamo Chadema, CUF na CCM ambavyo vilidai kuwa vimekaguliwa na wakaguzi binafsi na kuwasilisha hesabu hizo katika Ofisi ya CAG.
Sakata hilo liliingiliwa kati na Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi aliposema kuwa hatazuia ruzuku ya vyama vya siasa kutokana na mkanganyiko wa ukaguzi uliojitokeza na kwamba kufanya hivyo itakuwa ni kukiuka sheria.
Uamuzi huo pia uliafikiwa na Kamati ya PAC ambayo awali, ilimwagiza Msajili huyo kusimamisha ruzuku hiyo hadi hapo vyama hivyo vitakapokuwa vimekaguliwa hesabu zao.
SOURCE:Mwananchi.co.tz

No comments: