KAMA Liverpool ikishinda mechi mbili tu kati ya
tatu ilizobakiza kufunga msimu huu wa Ligi Kuu England, basi historia
itaandikwa upya katika kurasa za ligi hiyo. Hakuna atakayeamini kwa
urahisi lakini itakuwa ndio hali halisi.
Ushindi wa mabao 3-2 ilioupata juzi Jumapili dhidi
ya Norwich City ugenini, umeiacha Liverpool ikiwa inaongoza kwa pointi
tano mbele ya Chelsea. Sasa hata kama Liverpool itafungwa na Chelsea,
lakini ikafanikiwa kushinda katika mechi dhidi ya Crystal Palace na
Newcastle United, itatawazwa kuwa mabingwa wapya wa England.
Kocha wa Liverpool, Brendan Rodgers, amesema
alitumia maneno ya kishujaa ya kiongozi wa kampeni za janga la
Hillsborough, Margaret Aspinall, kuwatia moyo wachezaji wake katika
ushindi huo dhidi ya Norwich.
Mtoto wa Aspinall, James, alifariki katika janga
hilo lililoua mashabiki 96 wa Liverpool katika pambano dhidi ya
Nottingham Forest mwaka 1989.
Aspinall alizungumza katika maadhimisho ya miaka
25 ya janga hilo uwanjani Anfield Jumanne iliyopita na Rodgers
aliyatumia maneno hayo katika pambano dhidi ya Norwich.
“Alituambia kuhusu kuzidiwa na mawazo. Mambo
yanaweza kuwa magumu, lakini unaweza kupigana sana na kushinda. Hayo
ndio maneno tuliyowaambia wachezaji wetu kabla ya mechi. Tuliyaandika
ukutani. Ni klabu ambayo kwa sasa wote sisi ni kitu kimoja. Wote
tunapigana kushinda jambo moja,” alisema Rodgers.
Ushindi dhidi ya Norwich pia uliihakikishia
Liverpool nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao, huku
kocha Rodgers akimsifu kinda Raheem Sterling, akisema ndiye kinda bora
zaidi barani Ulaya kwa sasa.
“Hapana shaka ndiye Mchezaji Chipukizi Bora zaidi
England kwa sasa. Nimefurahishwa na jinsi alivyopevuka. Anafanya kazi
kubwa uwanjani. Tumejaribu kumchezesha katika nafasi tofauti kutokana na
akili yake ya soka. Ni kijana mpole,” alisema.
SOURCE: Mwanaspoti.co.tz
SOURCE: Mwanaspoti.co.tz
No comments:
Post a Comment