Tuesday, 22 April 2014

LIVERPOOL YANG'ARA NYUMBANI, CHELSEA YATESA UGENINI

Vinara hao wa Ligi Kuu England, Liverpool jana Jumapili walidhihirisha kwamba wamepania kuubeba ubingwa wa ligi hiyo msimu huu baada ya kuichapa Man City mabao 3-2 katika mchezo mkali uliofanyika kwenye Uwanja wa Anfield.
STEVEN Gerrard alidondosha chozi, kisha akawaambia wenzake wameshamaliza kazi ya Manchester City na sasa kilichobaki ni kwenda kuichapa Norwich City kwao wakati kikosi chake cha Liverpool kikisonga taratibu kuelekea kwenye ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu vinara hao wa Ligi Kuu England, Liverpool jana Jumapili walidhihirisha kwamba wamepania kuubeba ubingwa wa ligi hiyo msimu huu baada ya kuichapa Man City mabao 3-2 katika mchezo mkali uliofanyika kwenye Uwanja wa Anfield.

Kosa la nahodha wa Man City, Vincent Kompany la kushindwa kuondosha mpira kwenye goli lake lilimpa nafasi kiungo Philippe Coutinho kufunga bao la ushindi kwenye dakika 78 na kuwafanya Liverpool kufikisha pointi 77 kwenye msimamo wa ligi hiyo. Ushindi huo unaiweka Liverpool kwenye nafasi nzuri zaidi ya kutwaa ubingwa msimu huu licha ya kwamba watahitaji kushinda mechi zao zote nne zilizobaki ikiwamo dhidi ya Chelsea itakayofanyika Anfield.
Liverpool ilianza kwa kasi sana na kupata bao mapema kupitia kwa Raheem Sterling, aliyewageuza geuza mabeki wa Man City kama chapati kabla ya kufumua shuti lililomshinda kipa Joe Hart na kwenda moja kwa moja wavuni kwenye dakika ya sita tu. Haikuwachukua muda mrefu Liverpool kuongeza bao la pili baada ya Martin Skrtel kuunganisha kwa kichwa mpira wa kona na kuifanya timu hiyo kwenda mapumziko ikiwa mbele kwa mabao 2-0.
Man City ilipata pigo kwenye kipindi cha kwanza baada ya kumpoteza kiungo wake, Yaya Toure kwa kuumia. Kipindi cha pili kilianza kwa kasi na Man City kuiweka Liverpool kwenye wakati mgumu kwa kusawazisha mabao kupitia kwa David Silva na Glen Johnson, aliyejifunga.
Wakati Man City wakiamini watapata walau pointi moja ugenini, beki wao Kompany, alifanya kosa kubwa kwa kushindwa kuokoa hatari iliyotokana na mpira wa kurusha na kumpa nafasi Coutinho kufunga bao la ushindi.
Kwenye mchezo huo, kiungo Jordan Henderson alitolewa kwa kadi nyekundu na mwamuzi Mark Clattenburg baada ya kumchezea rafu Samir Nasri.
Mchezo mwingine wa ligi hiyo, Chelsea ikiwa ugenini kwa Swansea City waliendelea kung’ang’ania kwenye mbio za ubingwa baada ya kushinda bao 1-0, shukrani kwa bao la straika, Demba Ba.
Ba amezidi kung’ara baada ya kufunga tena bao muhimu Chelsea kama alivyofanya wiki iliyopita walipomenyana na PSG kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya alipofunga bao muhimu. Chelsea sasa imefikisha pointi 75 na kushika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi hiyo.
SOURCE: Mwanaspoti.co.tz

No comments: