Tuesday, 22 April 2014

IKO WAZI UKWELI HAUJIFICHI

STRAIKA, Wayne Rooney, amesema hana kitu kingine zaidi ya kupendezwa na soka la staa wa Liverpool, Luis Suarez na kwamba atakuwa na heshima kubwa kwa mahasimu wao hao kama watatwaa taji la Ligi Kuu England msimu huu, Rooney na kikosi chake cha Manchester United jana Jumapili walitarajia kumenyana na Suarez kwenye mchezo wa ligi hiyo uwanjani Old Trafford.

Msimu huu Suarez amekuwa kwenye ubora mkubwa akiwa amefunga mabao 24 na kupika mengine 10 katika mechi 23 alizocheza kwenye Ligi Kuu England kabla ya jana kumenyana na Man United. Staa huyo wa Uruguay alikosa mechi za mwanzoni mwa msimu kwa kuwa alikuwa amefungiwa mechi sita kutokana na kosa la kumng’ata beki wa Chelsea, Branislav Ivanovic.
Rooney alizungumzia matukio ya utata ya Suarez, lakini baadaye alikiri kukubali uwezo wa mchezaji huyo kuwa upo juu.
“Watu wanasema Suarez ni mwanasoka wa mtaani kama mimi, lakini ninavyoona alipokulia yeye huko Uruguay palikuwa pagumu zaidi ya nilipokulia mimi Liverpool,” alisema Rooney.
“Kila anayefahamu mpira anaweza kumwona jinsi Suarez anavyopambana na kuwa na moyo wa kutaka ushindi. Anafanya kila kitu kuhakikisha anafanikiwa. Anaweza kuwa na makosa mengi, lakini kwenye suala la kuwa mwanasoka, sina kitu kingine zaidi ya kumkubali tu.”
Liverpool ilikwenda Old Trafford ikiwa mbele kwa pointi 11 dhidi ya Man United na ipo kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu, kitu ambacho Rooney alisema atakuwa na heshima kubwa kwa mahasimu wao hao kama wataibuka mabingwa msimu huu.
Alisema: “Kama Liverpool itatwaa ubingwa, litakuwa ni suala la timu bora kwenye nchi hii. Kwenye klabu yetu ya Man United hakuna atakayependa, lakini lazima wataheshimu mafanikio ya wapinzani wao.”

TEMBO ATWAA TUZO YA MWANASOKA BORA AFRIKA

KIUNGO, Yaya Toure, amechaguliwa kuwa Mwanasoka Bora wa Mwaka wa Afrika ikiibuka kwa mara ya tatu mfululizo na kuwabwaga mastaa kadhaa akiwamo Mnigeria, John Obi Mikel.
Kwenye tuzo zilizofanyika mjini Lagos, Nigeria juzi Alhamisi usiku, kiungo huyo wa Manchester City alimpiku staa mwenzake straika, Didier Drogba ambaye ni  mchezaji wa zamani wa klabu ya chelsea ya na timu ya taifa ya Ivory Coast
Kwa kutwaa tuzo kwa miaka mitatu mfululizo, jambo hilo limemfanya Toure, 30, kufikia rekodi za Abedi Pele na Samuel Eto’o waliowahi kufanya hivyo huko nyuma.
Mikel ameshindwa kumshinda Yaya Toure na kuifariji Nigeria ambayo mara ya mwisho kwa nyota wake kutwaa tuzo hiyo ilikuwa mwaka 1999 wakati fowadi, Nwankwo Kanu, alipoibuka kidedea.
Yaya Toure alikuwa mchezaji muhimu wa Ivory Coast wakati walipotinga robo fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka jana na mbio za kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika Brazil mwaka huu, lakini Mikel alikuwa akipewa nafasi pia kutokana na kuisaidia Nigeria kutwaa ubingwa wa Afrika na kufuzu Kombe la Dunia.
Tuzo nyingine zilitolewa kwa Stephen Keshi (Kocha Bora) na kiungo wa Misri, Mohamed Aboutrika (Mwanasoka Bora wa Soka la Ndani)  huku tuzo ya gwiji la Afrika ikinyakuliwa na kocha, Bruno Metsu, ambaye kwa sasa ni marehemu.


LIVERPOOL YANG'ARA NYUMBANI, CHELSEA YATESA UGENINI

Vinara hao wa Ligi Kuu England, Liverpool jana Jumapili walidhihirisha kwamba wamepania kuubeba ubingwa wa ligi hiyo msimu huu baada ya kuichapa Man City mabao 3-2 katika mchezo mkali uliofanyika kwenye Uwanja wa Anfield.
STEVEN Gerrard alidondosha chozi, kisha akawaambia wenzake wameshamaliza kazi ya Manchester City na sasa kilichobaki ni kwenda kuichapa Norwich City kwao wakati kikosi chake cha Liverpool kikisonga taratibu kuelekea kwenye ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu vinara hao wa Ligi Kuu England, Liverpool jana Jumapili walidhihirisha kwamba wamepania kuubeba ubingwa wa ligi hiyo msimu huu baada ya kuichapa Man City mabao 3-2 katika mchezo mkali uliofanyika kwenye Uwanja wa Anfield.

Kosa la nahodha wa Man City, Vincent Kompany la kushindwa kuondosha mpira kwenye goli lake lilimpa nafasi kiungo Philippe Coutinho kufunga bao la ushindi kwenye dakika 78 na kuwafanya Liverpool kufikisha pointi 77 kwenye msimamo wa ligi hiyo. Ushindi huo unaiweka Liverpool kwenye nafasi nzuri zaidi ya kutwaa ubingwa msimu huu licha ya kwamba watahitaji kushinda mechi zao zote nne zilizobaki ikiwamo dhidi ya Chelsea itakayofanyika Anfield.
Liverpool ilianza kwa kasi sana na kupata bao mapema kupitia kwa Raheem Sterling, aliyewageuza geuza mabeki wa Man City kama chapati kabla ya kufumua shuti lililomshinda kipa Joe Hart na kwenda moja kwa moja wavuni kwenye dakika ya sita tu. Haikuwachukua muda mrefu Liverpool kuongeza bao la pili baada ya Martin Skrtel kuunganisha kwa kichwa mpira wa kona na kuifanya timu hiyo kwenda mapumziko ikiwa mbele kwa mabao 2-0.
Man City ilipata pigo kwenye kipindi cha kwanza baada ya kumpoteza kiungo wake, Yaya Toure kwa kuumia. Kipindi cha pili kilianza kwa kasi na Man City kuiweka Liverpool kwenye wakati mgumu kwa kusawazisha mabao kupitia kwa David Silva na Glen Johnson, aliyejifunga.
Wakati Man City wakiamini watapata walau pointi moja ugenini, beki wao Kompany, alifanya kosa kubwa kwa kushindwa kuokoa hatari iliyotokana na mpira wa kurusha na kumpa nafasi Coutinho kufunga bao la ushindi.
Kwenye mchezo huo, kiungo Jordan Henderson alitolewa kwa kadi nyekundu na mwamuzi Mark Clattenburg baada ya kumchezea rafu Samir Nasri.
Mchezo mwingine wa ligi hiyo, Chelsea ikiwa ugenini kwa Swansea City waliendelea kung’ang’ania kwenye mbio za ubingwa baada ya kushinda bao 1-0, shukrani kwa bao la straika, Demba Ba.
Ba amezidi kung’ara baada ya kufunga tena bao muhimu Chelsea kama alivyofanya wiki iliyopita walipomenyana na PSG kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya alipofunga bao muhimu. Chelsea sasa imefikisha pointi 75 na kushika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi hiyo.
SOURCE: Mwanaspoti.co.tz

BAADA YA MIAKA 20 YA KUFULIA SASA UBINGWA HUOOO

KAMA Liverpool ikishinda mechi mbili tu kati ya tatu ilizobakiza kufunga msimu huu wa Ligi Kuu England, basi historia itaandikwa upya katika kurasa za ligi hiyo. Hakuna atakayeamini kwa urahisi lakini itakuwa ndio hali halisi.
Ushindi wa mabao 3-2 ilioupata juzi Jumapili dhidi ya Norwich City ugenini, umeiacha Liverpool ikiwa inaongoza kwa pointi tano mbele ya Chelsea. Sasa hata kama Liverpool itafungwa na Chelsea, lakini ikafanikiwa kushinda katika mechi dhidi ya Crystal Palace na Newcastle United, itatawazwa kuwa mabingwa wapya wa England.
Kocha wa Liverpool, Brendan Rodgers, amesema alitumia maneno ya kishujaa ya kiongozi wa kampeni za janga la Hillsborough, Margaret Aspinall, kuwatia moyo wachezaji wake katika ushindi huo dhidi ya Norwich.
Mtoto wa Aspinall, James, alifariki katika janga hilo lililoua mashabiki 96 wa Liverpool katika pambano dhidi ya Nottingham Forest mwaka 1989.
Aspinall alizungumza katika maadhimisho ya miaka 25 ya janga hilo uwanjani Anfield Jumanne iliyopita na Rodgers aliyatumia maneno hayo katika pambano dhidi ya Norwich.
“Alituambia kuhusu kuzidiwa na mawazo. Mambo yanaweza kuwa magumu, lakini unaweza kupigana sana na kushinda. Hayo ndio maneno tuliyowaambia wachezaji wetu kabla ya mechi. Tuliyaandika ukutani. Ni klabu ambayo kwa sasa wote sisi ni kitu kimoja. Wote tunapigana kushinda jambo moja,” alisema Rodgers.
Ushindi dhidi ya Norwich pia uliihakikishia Liverpool nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao, huku kocha Rodgers akimsifu kinda Raheem Sterling, akisema ndiye kinda bora zaidi barani Ulaya kwa sasa.
“Hapana shaka ndiye Mchezaji Chipukizi Bora zaidi England kwa sasa. Nimefurahishwa na jinsi alivyopevuka. Anafanya kazi kubwa uwanjani. Tumejaribu kumchezesha katika nafasi tofauti kutokana na akili yake ya soka. Ni kijana mpole,” alisema.
SOURCE: Mwanaspoti.co.tz

Wednesday, 16 April 2014

UPINZANI WASUSIA VIKAO VYA BUNGE LA KATIBA TZ

Baadhi ya wajumbe wa Bunge Maalum la Rasimu ya Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wameondoka kwa hasira katika kikao cha bunge hilo kinachoendelea mjini Dodoma.
Hasira yao inatokana na madai kwamba maoni ya wananchi yaliyowasilishwa na Tume ya Marekebisho ya Katiba Mpya yamekuwa yakipuuzwa.
Wajumbe wa bunge hilo ambao ni kutoka upande wa upinzani chini ya umoja unaojulikana kama UKAWA, yaani Umoja wa Katiba ya Wananchi, wameamua kutoka nje kupinga kile wanachosema ni kupuuzwa kwa makusudi maoni ya wananchi wanaotaka muungano wa muundo wa serikali tatu kama yalivyopendekezwa katika rasimu ya katiba hiyo.

  

 

Kilio cha mwananchi

Akichangia katika kikao cha bunge hilo Jumatano jioni, mmoja wa wajumbe Profesa Ibrahim Lipumba amelalamikia kauli za ubaguzi zinazotolewa na baadhi ya wajumbe, hususan wanaotaka muundo wa muungano wa serikali mbili, alieleza sababu za kutaka serikali tatu kuwa zitasaidia kutatua matatizo yaliyopo katika muundo wa sasa.
Hata hivyo hakusita kupinga kile anachokiita kauli za ubaguzi kutoka kwa wajumbe wanaopinga mawazo ya wachache bungeni humoi.
"Hatuwezi kuwa kama kundi la wapiganaji linalohamamisha ubaguzi ndani ya Tanzania, hili hatulikubali, hatulikubali, hatulikubali, watu wote tunaotaka katiba ya wananchi tunawaachia muendelee na kikao chao.Ahsanteni sana".
Mara baada ya kusema hivyo, wajumbe waliounga mkono kauli yake waliinuka na kutoka nje.
Hata hivyo, kikao cha bunge hilo kiliendelea baada ya makamu mwenyekiti wa bunge hilo kusema idadi ya wajumbe waliobaki walitosha kuendelea na kikao hicho.

Muundo wa serikali

Wanaounga mkono muundo wa serikali tatu, wanasema muundo wa sasa wa serikali mbili umeshindwa kutatua masuala yenye mgogoro katika muungano, maarufu kama kero za muungano, hivyo kudhoofisha muungano huo.
Hata hivyo wajumbe wanaounga mkono serikali mbili, yaani serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar wanasema muundo wa serikali tatu ni kuvunja muungano wa Tanganyika na Zanzibar na pia itakuwa gharama kuiendesha serikali ya tatu.
Bunge hilo lenye zaidi ya wajumbe mia sita linaundwa na wabunge wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Baraza la wawakilishi Zanzibar na wajumbe 201 walioteuliwa na rais wa Tanzania kutoka makundi mbalimbali ya kijamii.Wajumbe 191 kutoka upinzani walitoka nje ya bunge kupinga mwenendo wa bunge hilo katika kujadili rasimu ya katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
SOURCE: BBCSwahili.com

AJALI YA MELI YATIKISA DUNIA

Zaidi yawatu 300 hawajapatikana baada ya meli iliyowabeba wanafunzi kuzama nchini Kore Kusini, awali maafisa walikuwa wamesema kuwa wengi wa abiria waliokuwa katika meli hiyo waliokolewa.
"Kwa kweli kulikuwa na sauti kubwa na meli ghafla ikaanza kuegemea upande mmoja," amesema abiria aliyeokolewa, Kim Song-Muk.
"watu walikuwa wakihangaika kukimbilia maeneo ya juu ya meli, lakini ilikuwa vigumu kufanya hivyo kutokana na meli kupinduka."
Bado haijafahamika kilichosababisha kuzama kwa meli hiyo, ambayo kwa kiasi kikubwa iliwabeba wanafunzi wa shule, lakini watu walionusurika katika ajali hiyo wanatoa maelezo sawa kuhusu tukio hilo la kutisha.
Kikosi cha Walinzi wa Pwani ya Korea Kusini kimesema abiria wapatao mia tatu hawajulikani walipo baada ya meli kupinduka na kuzama.
Watu wawili wamefahamika kupoteza maisha na watu mia moja na sitini na wanne wameokolewa.
Wengi wa abiria wa meli hiyo walikuwa wanafunzi wa sekondari wakiwa katika safari ya masomo kuelekea kisiwa cha Jeju, nchini Korea Kusini.
Meli hiyo ilikuwa na watu 460, Zaidi ya miatatu hawajapatikana , wengine 164 wameokolewa na wengine wawili wamethibitishwa kufariki.
SOURCE: BBC Swahili.com

NYOTA ALIYEING'ARISHA TIMU YA POOL TABLE MZUMBE MBEYA

 Mchezaji Sudi Mlela al maarufu kama "Dr.kingshot" kutoka timu ya chuo kikuu Mzumbe kampasi ya Mbeya aliibuka kuwa nyota wa mchezo wa mashindano ya pool table safari lager wakati wa fainali kati ya timu ya Mzumbe University Mbeya na Mbeya University of science and technology (MUST), Dr.kingshot aliibuka nyota baada ya kuweza kuipatia ushindi timu ya chuo kikuu Mzumbe Mbeya kutokana na kucheza katika kizuri kilichopelekea mchezaji wa timu ya MUST kushindwa kumaliza mchezo mapema ingawa alipata nafasi ya kucheza mpira mweusi (black ball) zaidi ya mara tano na kushindwa kupeleka mpira huo shimoni kutokana na kiwango cha mchezo alichokuwa akicheza Dr.kingshot wakati wa mchezo huo kuwa cha hali ya juu na hatimaye Dr.kingshot akafanikiwa kuipatia timu yake ya Mzumbe Mbeya goli la 13 dhidi ya magoli 12 yaliyofungwa na MUST wakati wa fainali na kuifanya timu yake kuibuka washindi wa mashindano hayo.

Tuesday, 15 April 2014

IKULU YAONYESHA HATI YA MUUNGANO

Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue akizungumza Ikulu jana, alisema madai ya kuonyeshwa kwa Hati ya Muungano yalianza siku nyingi na hawakufahamu kama yangefika hatua yalipofikia.
“Ukweli ni kuwa hati hiyo ipo na ilikuwapo siku zote,” alisema Balozi Sefue na kuongeza: “Hata hivyo, tukubaliane kwamba kuna hati fulani ambazo ni kiini cha uwepo wetu kama Taifa huru, kama Jamhuri huru, kama Muungano huru ambazo zinahifadhiwa kama mboni ya jicho.
Balozi Sefue alizitaja kuwa ni Hati ya Uhuru wa Tanganyika ya mwaka 1961, Hati ya Tanganyika kuwa Jamhuri mwaka 1962 na Hati ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ya mwaka 1964 na kusema zinahifadhiwa maeneo maalumu ili zisipotee au kuharibika.
“Maneno yamekuwa mengi mno, tuhuma zimekuwa nyingi, dhihaka zimekuwa nyingi kiasi cha wananchi kuanza kutia shaka kuwa hati ya Muungano ipo au la,” alisema na kuongeza:
“Kutokana na agizo na ridhaa ya Rais Jakaya Kikwete, ninaleta kwenu waandishi wa habari hati halisi ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar iliyotiwa saini Zanzibar na waasisi wetu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Abeid Aman Karume ili muione, mridhike nayo na muwajulishe wananchi.”
Baada ya kuwaonyesha aliwagawia wanahabari hao nakala ya hati hiyo na kusema Ikulu itafanya utaratibu wa kuiweka katika makumbusho ya Taifa ili kila mwananchi anayependa kuiona aende huko.
Kuhusu hati hiyo kupelekwa bungeni mjini Dodoma, Balozi Sefue alisema iwapo Mwenyekiti wa Bunge la Katiba, Samuel Sitta ataiomba, Ikulu itaipeleka ili kuondoa mjadala wa uwepo wa hati hiyo.
“Tumesikitishwa, kusononeka na kufadhaika sana na tuhuma nzito kwamba waasisi wetu hawakuwa makini au walitufanyia kiini macho. Hatukutarajia Watanzania wenzetu wafikie hapo ni jambo zito,” alisema Balozi Sefue
Katika kipindi cha maswali, Balozi Sefue alishindwa kubainisha ilikuwa wapi wakati wote na kusisitiza: “Kazi ya leo ilikuwa ni kuwaonyesha hati hiyo na ninaomba maswali yenu yajikite katika hili.
 SOURCE: Mwananchi.co.tz

BOMU LALIPUKA ARUSHA

Tukio hilo lilitokea jana saa mbili usiku wakati mamia ya watu wakiwa katika baa hiyo wakiangalia mechi ya soka ya Ligi Kuu ya England kati ya Chelsea na Swansea. Chelsea ilishinda 1-0.
Watu kadhaa wamejeruhiwa kutokana na mlipuko unaodhaniwa kuwa ni wa bomu katika baa maarufu ya Arusha Night Park katika eneo la Mianzini katika jiji la Arusha.Tukio hilo lilitokea jana saa mbili usiku wakati mamia ya watu wakiwa katika baa hiyo wakiangalia mechi ya soka ya Ligi Kuu ya England kati ya Chelsea na Swansea. Chelsea ilishinda 1-0.  Mmoja wa wamiliki wa baa hiyo, Angelo Mwoleka pia alithibitisha kutokea mlipuko huo na kueleza kujeruhiwa watu kadhaa.
“Ni kweli kuna mlipuko umetoka na watu kujeruhiwa, mimi sikuwepo ila nipo njiani nakwenda eneo la tukio, “alisema. Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, John Lymo alisema watu saba waliumia vibaya kutokana na bomu hilo na walipelekwa katika Hospitali ya Mkoa Arusha ya Mount Meru.Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus (pichani), alisema: “Hivi sasa tunaendelea na uokoaji na uchunguzi umeanza.”

Tukio hilo limekuja wakati bado jiji la Arusha likiwa na kumbukumbu ya kushambuliwa kwa mabomu kwa Kanisa la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi lililopo eneo la Olasiti na jingine Uwanja wa Soweto wakati Chadema walipokuwa wakifunga kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani. Katika matukio yote hayo, watu sita waliuawa na wengi kujeruhiwa

SOURCE: Mwananchi.co.tz

WASHIRIKI BORA WA MASHINDANO YA POOL TABLE SAFARI LAGER JIJINI MBEYA


       Amina Muhina, mwanadada kutoka chuo kikuu Mzumbe Mbeya ni msichana pekee aliyeonyesha kiwango cha juu na kuwashinda wasichana wenzake kutoka vyuo vishiriki katika mashindano ya safari lager pool table, Amina Muhina alionyesha ufundi na umahiri wa kumiliki mpira wakati wa mchezo huo na alifanikiwa kuibuka mchezaji bora kwa upande wa wasichana na kujishindia kiasi cha sh.100,000/= pamoja na nafasi ya kushiriki mashindano ya mchezo wa meza kwa ngazi ya kitaifa mkoani Kilimanjaro mwaka huu kama msichana pekee kutoka mkoani Mbeya.
      Steven Mussa al maarufu kama "Kanumba au Zombi" mshiriki kutoka chuo kikuu Mzumbe kampasi ya Mbeya aibuka kuwa kivutio kikubwa kwa wachezaji na watazamaji wa michuano hiyo baada ya kuonyesha kiwango cha juu na kujishindia shilingi 150,000/= kitu ambacho hakuna mshiriki wa kiume aliyeweza kuonyesha kiwango cha juu wakati wa mashindano hayo pia alifanikiwa kuibuka mchezaji bora wa kiume wa mashindano hayo kwa kuwafunga wachezaji wenzake kutoka vyuo vingine Magoli mawili kwa kila mpinzani wake kwa kila michezo mitatu waliyopangiwa kucheza kitu kilichomfanya aonekane kivutio kikubwa miongoni mwa wachezaji wenzake.

YALIYOJIRI KATIKA MASHINDANO YA SAFARI LAGER POOL TABLE JIJINI MBEYA

Mashindano ya mchezo wa meza (pool table) ya bia ya safari lager yaliyofanyika tarehe 13 Aprili 2014 katika viwanja vya Airport Pub yalitawaliwa na matukio mbalimbali yaliyosababisha michuano hiyo kuchukua muda mrefu kuanzia majira ya saa sita mchana mpaka saa tisa usiku ambapo timu ya chuo kikuu Mzumbe kampasi ya mbeya  kuibuka washindi wa mashindano hayo
  Mnamo majira ya  saa 12:50 mchana ilitokea hitilafu ya umeme uliokuwa umetokana na Umeme wa jenereta hitilafu iliyosababisha moto kulipuka, tukio lililosababisha watu kukimbilia nje ya ukumbi wa Airport Pub na mashindano kusimama kwa muda, Licha ya jitihada ya kupatikana kwa jenereta lingine lakini umeme ulifanikiwa kurudishwa majira ya saa nane mchana, tukio la kukatika umeme liliendelea tena kutokea majira ya saa tisa usiku wakati timu ya chuo kikuu Mzumbe ikicheza fainali na timu ya  "MUST" hali iliyoleta tafrani ya hapa na pale kwa timu shiriki.
Mnamo majira ya saa tisa mchana wakati wakicheza timu nya chuo cha TIA na timu ya chuo kikuu MUST amabapo mchezaji kutoka timu ya MUST aligundulika akitumia kitambulisho batili cha kufanyia mitihani badala ya kitambulisho cha chuo, mzozo huo ulifanikiwa kumalizwa na mwenyekiti wa chama cha mpira wa meza mkoa wa Mbeya  Bw. Aaron Samuel.
  Mzozo mwingine ulitokea wakati wakicheza timu za TIA na MUST baada ya kubainika meza waliyokuwa wakitumia kutokuwa na ubora, hali iliyosababisha wachezaji kushindwa kucheza kwa kiwango amabapo mipira ilikuwa inakimbilia kuingia kwenye shimo ambalo siyo chaguo la mchezaji pia hali hiyo ilipelekea wachezaji hao kubeba meza hiyo na kuipeleka nje kwa ajili ya kuendelea ana mashindano ingawa tatizo hilo halikupata ufumbuzi kitu kilichosababisha meza hiyo kugomewa na wachezaji baadaye hivyo zilitumia meza mbili badala ya tatu


Monday, 14 April 2014

HATIMAYE MZUMBE UNIVERSITY MBEYA CAMPUS WAIBUKA WASHINDI

      Timu ya mchezo wa meza (pool table) ya Mzumbe University Campus ya Mbeya iliibuka mshindi wa mashindano ya safari lager pool table yaliyofanyika jana tarehe 13 Aprili 2014 kwenye viwanja vya Airport pub jijini mbeya mashindano yaliyojumuisha timu tano za vyuo vikuu kutoka jijini Mbeya.
Ushindi huo umeipa nafasi timu ya mpira wa meza ya chuo kikuu Mzumbe kampasi ya Mbeya kwenda kushiriki mashindano kwa ngazi ya kitaifa yatakayofanyika mwishoni mwa mwezi huu mkoani Kilimanjaro wilaya ya Moshi mjini, mashindano yatakayo shirikisha timu zilizofuzu kutoka kila mkoa nchini.
Timu ya mchezo wa meza ya chuo kikuu Mzumbe mbeya inajumuisha wachezaji nane, wa kiume saba na wa kike mmoja, timu imefanikiwa kushinda nafasi mbalimbali licha ya kutwaa ushindi wa mkoa.
    Mchezaji Steven Mussa Kyasi al maarufu kama "Kanumba au Zombi" alifanikiwa kutwaa ushindi wa mchezaji bora wa  kiume na kujinyakulia fedha taslimu sh.150,000/=, mchezaji Amina Muhina naye alifanikiwa kushinda nafasi ya mchezaji bora wa kike na kujinyakulia kitita cha sh.100,000/=, huku Mchezaji Sudi Mlela al maarufu kama "Dr.king shot" alifanikiwa kuiwezesha timu yake kushinda mchezo huo.
Timu ya chuo kikuu Mzumbe Mbeya baada ya kushinda  nafasi ya kwanza ilijinyakulia fedha taslimu sh.500,000/=, nafasi ya pili ilishikiliwa na timu  ya Mbeya University of science and technology (MUST), nafasi ya tatu ilishikiliwa na timu ya Tanzania Institute of Accountancy (T.I.A).
 Mashindano ya mchezo wa meza yanadhaminiwa na TBLchini ya bia ya safari lager, mashindano hayo yalisimamiwa na mwenyekiti wa chama cha mchezo wa meza mkoa wa mbeya Bw. Aaron Samuel na mweka hazina kutoka chama cha mpira wa meza nchini Bw.Wito Mwandunga.

Friday, 11 April 2014

MAZOEZI YA KUJIANDAA NA MASHINDANO YA POOL TABLE VYUO VIKUU TANZANIA

         Wachezaji wa timu ya mchezo wa meza (pool table) chuo kikuu Mzumbe kampasi ya Mbeya wakiwa wanajiandaa na mashindano ya mchezo wa meza kwa  ngazi ya mkoa yanayotarajiwa kufanyika wikiendi hii ndani ya jiji la Mbeya katika viwanja vya Airport Pub.
Kwa mujibu wa kaptain aliyemaliza muda wake wa timu hiyo ya chuo kikuu Mzumbe kampasi ya Mbeya anayefahamika kwa jina la Kelvin Mwita (a.k.a Kevoo) timu hiyo inajumuisha wachezaji nane (8) wakiwemo wachezaji wa kiume saba (7) na wa kike mmoja(1) anayejulikana kwa jina la Amina Muhina.
  Maandaliizi ya timu yao yanaendelea vizuri na wapo tayari kushiriki na kuchukua ubingwa wa mashindano hayo yanayo dhaminiwa na kampuni ya bia Tanzania TBL kupitia bia yao ya safari lager wakishirikiana na chama cha mchezo wa meza Tanzania (TANZANIA POOL ASSOCIATION).
  Mashindano hayo yatafanyika jijini Mbeya mnamo tarehe 13 Aprili 2014 na yata jumuisha timu kutoka vyuo vikuu vitano vilivyopo ndani ya jiji la Mbeya.
 Timu ya chuo kikuu Mzumbe kampasi ya Mbeya kwa sasa watashiriki kwa mara ya nne katika mashindano haya, kwa mara ya kwanza mwaka 2011 waliibuka washindi wa pili kwa ngazi ya mkoa, kwa mara ya pili waliibuka washindi wa pili na kwa mara ya tatu mwaka 2013 waliibuka washindi wa kwanza kwa ngazi ya mkoa na washindi wa pili ngazi ya kitaifa.
 Timu ya mchezo wa meza (pool table) ya chuo kikuu Mzumbe kampasi ya Mbeya inaahidi ushindi katika ngazi zote kimkoa na kitaifa, mashindano ya kitaifa yatafanyika mapema mwaka huu ndani ya mkoa wa kilimanjaro wilaya ya Moshi mjini.



MAUAJI NA GHASIA JIJINI MBEYA

Leo tarehe 11 Aprili 2014 majira ya saa nne asubuhi jiji la Mbeya liligeuka kuwa uwanja wa maapambano kati ya jeshi la polisi na madereva wa boda boda jijini humo. Ghasia hizo zimetokana na mauaji yaliyotokea jijini hapo ya mmoja wa dereva wa boda boda ambaye kifo chake kimesababishwa na wivu wa kimapenzi.
         Marehemu ambaye alikuwa miongoni mwa madereva wa boda boda katika kituo cha mafiati jijini hapo aliuwawa na watu wasiojulikana baada ya kuchomwa na kitu chenye ncha kali na kujeruhiwa sehemu mbali mbali za mwili wake.
        Taarifa kutoka kwa  Khalfan Lusinga, 21 anayefanya kazi ya kuosha magari eneo la mafiati jijini Mbeya anadai kuwa kifo cha marehemu kimetokana na wivu wa kimapenzi unaomuhusisha marehemu na mwanamke aliyekuwa mke wa marehemu kabla ya ndoa yao kutengana.
         Mwanamke huyo amekamatwa leo baada ya kikundi cha madereva wa boda boda kuungana na kutaka kumuua mwanamke huyo kwa lengo la kulipiza kisasi cha kifo cha dereva mwenzao, polisi mkoani mbeya walifanikiwa kufika eneo la tukio maeneo ya Mwanjelwa kabla ya madereva hao kutimiza azma yao ya kutaka kumuua mwanamke huyo.
        Polisi mkoani humo walifanikiwa kuokoa maisha ya mwanamke huyo ambaye alikuwa tayari mikononi mwa madereva wa boda boda hao. kutokana na hatua hiyo madereva wa boda boda walianzisha ghasia za kutaka kupambana na jeshi la polisi kwa lengo la kutaka warudishiwe mwanamke aliyeokolewa na jeshi la polisi. tukio hili limetokea leo jijini Mbeya na kusababisha jeshi la polisi kutumia mabomu ya machozi ili kutuliza ghasia hizo zilizodumu kwa takribani masaa manne.

MFAHAMU MSHINDI WA TUZO YA HALL OF FAME 2014

    Baraka A. Dishon ni mwandishi wa mashairi na vitabu kwa lugha ya kiswahili na kiingereza, Alianza kazi ya uandishi wa mashairi na vitabu akiwa anasoma shule ya msingi, pia  alijifunza uandishi kupitia kwa Mama yake Mzazi ambaye alikuwa mwalimu wa shule ya msingi na mwandishi wa mashairi mbali mbali.
Baraka A. Dishon alianza kujulikana kupitia mashindano ya UMITASHUMTA akiwa darasa la tano mwaka 1998 katika shule ya  msingi Sambanyasoko, iliyopo wilaya ya Tarime mkoani Mara, aliposhiriki katika mashindano ya uandishi wa mashairi na kufanikiwa kuingia ngazi ya mkoa na baadae ngazi ya kitaifa ambapo alishindwa kushiriki ngazi ya kitaifa kutokana na kukosa wafadhili.
    Mnamo mwaka 2001 alijiunga shule ya sekondari Misonga ambapo aliendeleza kipaji chake cha uandishi wa mashairi alikuwa akitunga mashairi yenye mada tofauti kwa ajili ya kuwaelimisha wanafunzi wenzake nyakati za Asubuhi wakiwa Mstarini wakisubiri kuingia madarasani.
    Mwaka 2004 akiwa mwanafunzi shuleni hapo alipata nafasi ya kwenda kushiriki mashindano ya uandishi wa mashairi Nairobi nchini Kenya, mashindano yaliyohusisha shule zilizo chini ya Madhehebu ya kikristo Afrika Mashariki, alifanikiwa kuibuka mshindi wa tatu(3) katika uandishi wa mashairi na kushika nafasi ya kwanza kama Mwandishi bora wa Makala ya kiingereza.
   Mwaka 2005 alijiunga na shule ya Ufundi Musoma kwa ajili ya  kidato cha tano na sita katika mchepuo wa HKL, akiwa shuleni hapo alishiriki mashindano ya uandishi wa mashairi  yaliyoshirikisha shule za sekondari ikiwamo shule ya wasichana Kowaki na aliibuka mshindi wa kwanza kwa uandishi wa mashairi na makala.

   Mwaka 2006 alishiriki mashindano ya mazingira yaliyoratibiwa na ofisi ya Makamu wa Rais na alifanikiwa kushika nafasi ya kwanza na kutwaa tuzo ya mwandishi bora wa mazingira mwaka 2006.
   Mwaka 2009 aliajiriwa kama Mwalimu katika shule ya sekondari Morombe akiwa shuleni hapo kama mwalimu alifanikiwa kuanzisha kikundi cha wanafunzi wanaoandika mashairi kinachoitwa UJIKO GROUP.
  Mwaka 2011 alijiunga na chuo na chuo kikuu Mzumbe  kampasi ya Mbeya kusomea Shahada ya Sheria, akiwa chuoni hapo amefanikiwa kuandika mashairi mbali mbali ikiwamo shairi linalojulikana kwa jina la "Tatizo nini wanasheria". 
  Mnamo Aprili 2014 alipata taarifa ya mashindano ya tuzo za Hall of fame akiwa darasani  anandaa shairi kwa ajili ya sherehe ya Siku ya Wanasheria iliyofanyika tarehe 5 Aprili 2014 chuo kikuu Mzumbe kampasi ya Mbeya.
  Baraka A.Dishon aliibuka mshindi wa tuzo za Hall of fame katika kipengele cha mwandishi bora wa mashairi anayechipukia (Best Young Writer 2014) na kutwaa tuzo ya Shaaban Robert.

MSHINDI WA TUZO YA SHAABAN ROBERT MWAKA 2014

 Mwandishi Bora Wa Mashairi Tanzania 2014
Baraka Alfred Dishon, miaka 27, mwanafunzi wa sheria mwaka wa tatu chuo kikuu Mzumbe campus ya Mbeya, Aliibuka kuwa mshindi wa tuzo ya Shaban Robert katika kipengele cha mwandishi bora anayechipukia 2014 (Best Young Writer 2014), kupitia shairi aliloandika la "Katiba ni itakayo". Hall of Fame ni shindano linalo fanyika kila mwaka na linaloshirikisha vyuo vikuu vyote nchini Tanzania.

Moja ya sababu zilizomfanya Baraka .A. Dishon kuibuka mshindi wa tuzo hiyo ya Shaban Robert Best Young Writer 2014 ni uandishi wa kipekee aliounesha kwenye mashindano hayo kwa kuandika mashairi kwa lugha ya kiingereza yenye vina kitu ambacho hakuna mshiriki aliyewahi kutunga mashairi kwa lugha ya kiingereza.
Hall of fame ni mashindano yanayoshirikisha wanafunzi wenye vipaji mbalimbali kutoka vyuo vikuu nchini, mashindano haya yalianzishwa na Adam Antony ambaye ni mwanafunzi wa shahada ya sheria mwaka wa tatu chuo kikuu Mzumbe Morogoro.
  Mashindano ya tuzo za Hall of fame kwa mara ya kwanza yalishirikisha wanafunzi kutoka chuo kikuu Mzumbe pekee, kwa sasa baada ya mashindano hayo kufanyika zaidi ya miaka mitatu mfululizo mwaka 2015 tuzo za Hall of fame zitashirikisha wanafunzi kutoka vyuo vikuu mbalimbali Afrika Mashariki.

Tuesday, 8 April 2014

UKISTAAJABU YA MSEKWA UTAYAONA YA SITTA

Mh! Samwel Sitta Kikaangoni

Siku moja baada ya Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samwel Sitta kukiri kuchezewa kwa saini ya aliyekuwa Katibu wa Bunge la Tanganyika, Pius Msekwa na Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, Msekwa amesema, ‘mzungumzaji huyo ana lake jambo’.
 Utata huo ulianza wiki hii baada ya kamati za Bunge Maalumu la Katiba kuanza vikao vyake vya kujadili sura ya kwanza na ya sita ya Rasimu
Sitta akizungumza na gazeti hili juzi mjini Dodoma alisema ni kweli kuna maneno katika hati hiyo ya sheria namba 22 ya 1964, iliyosainiwa na Nyerere na Msekwa, Aprili 25, 1964, yameongezwa.
Alifafanua kuwa saini ya Nyerere imeongezwa herufi ‘us’ kwa kompyuta na katika sehemu ya saini ya Msekwa kumeandikwa neno ‘Msekwa’ kwa kompyuta, jambo ambalo ni makosa. Sitta alisema walioongeza maneno hayo ni wafanyakazi wa ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali baada ya kuona sehemu ya maandishi kwenye saini hizo hayasomeki, lakini walifanya makosa.
Msekwa akizungumza na gazeti hili jana alisema: “Saini iliyo katika hati original (halisi) ni ya kwangu mimi, lakini huyo anayesema zimechezewa muulizeni atakuwa na lake jambo. Kama kompyuta imekosea ni leo kwa kuwa kipindi hicho kompyuta hazikuwapo.”Aliongeza: “Ana lengo gani la kutilia shaka, ana lengo gani la kusema imechakachuliwa, kinachotakiwa ni hati original ambayo iko ofisi ya Katibu wa Bunge itolewe, kwanini tuendelee kuandikia mate wakati wino upo?”

MAJI HUFUATA MKONDO

Jimbo la chalinze lapata Mbunge Mpya
Mtoto wa Rais Kikwete, Ridhiwani akipiga kura jana wakati wa kura za maoni za CCM kupata mgombea ubunge Jimbo la Chalinze kwenye Shule ya Sekondari Msata jana. Picha na Julieth Ngarabali 
Katika uchaguzi huo, Ridhiwani aliongoza kwa kupata kura 758 na kuwabwaga wenzake watatu, aliyekuwa Mwenyekiti wa Yanga, Imani Madega aliyepata kura 335, Ramadhani Maneno (206) na Changwa Mohamed Mkwazu aliyepata kura 17
Mtoto wa Rais Jakaya Kikwete, Ridhiwani Kikwete ameibuka kidedea katika kinyang’anyiro cha kura za maoni za kuwania ubunge katika Jimbo la Chalinze, Mkoa wa Pwani.Katika uchaguzi huo, Kura tano ziliharibika.Uchaguzi huo unafanyika baada ya kifo cha aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Saidi Bwanamdogo kilichotokea Januari 22, mwaka huu.

WATANZANIA CHANGAMKIENI FURSA

Nafasi za Ajira 1,100 zatangazwa Leo Serikalini


Serikali kupitia Ofisi ya Rais Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma imetangaza nafasi za kazi 1,134 katika sekta mbalimbali za ofisi za umma Serikali kupitia Ofisi ya Rais Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma imetangaza nafasi za kazi 1,134 katika sekta mbalimbali za ofisi za umma.
Kwa mujibu wa Katibu wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, Xavier Daudi nafasi hizo za kazi ambazo zinapatikana katika tovuti ya Sekretarieti ya Ajira ya www.ajira.go.tz ni kwa ajili ya waajiri mbalimbali wa ofisi za umma. Katibu alifafanua kuwa nafasi 949 ni kwa ajili ya waajiri walioainishwa katika ofisi za wizara, halmashauri na nyingine 185 ni za taasisi na wakala mbalimbali za Serikali. Aidha, amewataka waombaji wote wa fursa za ajira kufungua matangazo yote mawili ya kazi na kuzingatia masharti ya Matangazo yote kama yalivyo katika lugha ya Kiingereza na Kiswahili kabla ya kutuma maombi yao Aprili 9, 2013.
SOURCE: Mwananchi.co.tz

KUTOA NI MOYO

JK aishukuru CRDB kusaidia Sh100mil kwa waathirika Moro

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akipokea hundi ya Sh100 milioni kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dk Charles Kimei (wa pili kushoto) kwa ajili ya kusaidia wananchi walioathirika na mafuriko mkoani Morogoro, hivi karibuni. Rais Kikwete alikabidhiwa hundi hiyo na Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB, Dk Charles Kimei katika shughuli fupi iliyofanyika Ikulu, Dar Es Salaam na kuhudhuriwa pia na viongozi mbalimbali akiwamo Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, mh.William Lukuvi, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia pia masuala ya maafa.

WAUZA SURA OUT!!

Wasanii wa muziki wa kizazi kipya Banana Zorro (kushoto) na Ray C (kulia) baada ya kutwaa tuzo za Kili Music Awards mwanzoni mwanzoni mwa mwaka 2007 
Kwa mujibu wa Basata na TBL, tuzo za mwaka huu zimefanyiwa mabadiliko katika mchakato wa kupata wateule watakaoingia katika vipengele mbalimbali.
SOURCE: Mwananchi.co.tz 

MABADILIKOYA HALI YA HEWA

Tatizo kwa jamii:  Angalia Shule iliyogeuka kuwa bwawa la samaki

www.kimsales.blogspot.com

Yala ni shule ya msingi iliyopo katika Kijiji cha Yala Kata ya Luhanga Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya na ipo umbali wa kilomita 40 kutoka Barabara Kuu ya Mbeya-Iringa, ili kufika shuleni hapo inakulazimu kutembea kwa mguu kutokana na magari na pikipiki kushindwa kufika Shule hiyo ina muda wa zaidi ya miaka 20 tangu kuanzishwa kwake, imezungukwa na mito minne ambayo imekuwa ikijaa maji kipindi cha masika na kusababisha kukatika kwa mawasiliano na ukosefu wa huduma mbalimbali ikiwa ni pamoja na elimu. Kutokana na tatizo hilo la mito kujaa maji shule hiyo imekuwa ikigeuka kuwa kisiwa na kusababisha wanafunzi na walimu kushindwa kufika shuleni kwani mito hiyo haina madaraja ya kuwawezesha kupita na kufika shuleni hapo. 
Wanafunzi wanaosoma katika shule hiyo wamekuwa wakitoka katika Vitongoji vya Mwashikamile, Ruaha, Waninyika, Mtakuja, Yala na Lusaka na wote hushindwa kuvuka mito hiyo na kufika shuleni huku walimu pia wakikumbwa na adha hiyo kutokana na shule hiyo kutokuwa na nyumba za kuishi Walimu.Jairos Mpale ni Mwenyekiti wa serikali ndogo ya maendeleo ya Mwashikamile katika Kijiji cha Yala anasema kuwa tatizo hilo limekuwa kubwa zaidi kwa mwaka huu ukilinganisha na miaka mingine
.Hii ni kutokana na mvua zinanyesha kwa wingi na wanafunzi wamekaa nyumbani muda mrefu bila kwenda shule.“Watoto wetu wameshindwa kwenda shuleni hapo tangu shule zote zilipofunguliwa Januari, kutokana na mito kujaa maji na kuna mamba wengi na viboko hivyo ni vigumu kuvuka kwenda katika Shule ya Yala na watoto wetu wamekosa masomo na hatujui ni lini wataanza masomo,” anasema.
SOURCE: Mwananchi.co.tz